UZINDUZI WA MFUKO WA MWANGOSI HAUWEZI KUWA TIBA!!!
NA EMMANUEL MKUWI
na mahitaji yake ili afahamu nini kinaendelea katika mazingira
yake, inaweza kuwa nyumbani, kazini, shuleni, kijijini na mtaani
kwake, nchini mwake n.k
Upatikanaji wa habari mhimu kwa mwanadamu zina umhimu wa pekee sana
ili kumfanya mbali na kufahamu kinachoendelea katika mazingira yake
lakini pia achukue tahadhari kulingana na habari hizo, hii inatokana
na ukweli kwamba mwanadamu kwa asili yake hana uwezo wa kufahamu jambo
lolote kama hajaambiwa au kuona.
Kutokana na umhimu huo wa kupata habari kama ilivyo ainishwa katika
ibara ya 18 ya katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania, serikali
ikaanzisha utaratibu wa kuhakikisha kwamba wananchi wake wanapata
fursa ya kutafuta kupata na kutoa habari kwa ajili ya mahitaji yao
mbalimbali ikiwemo maendeleo.
Utafutaji na upashaji wa habari hizo kwa ajili ya maendeleo ya
wananchi kwa mda mrefu sasa umeendelea kukabiliwa na changamoto
mbalimbali ambazo kwa kiwango kikubwa zinakwamisha jitihada za wana
habari katika utekelezaji wa majukumu yao na kufanya miongoni mwao
watekeleze kwa mashaka wajibu wao kwa jamii.
Changamoto hizo zinazo kwamisha wananchi kuhabarishwa, kuonywa,
kukosolewa, kuburudishwa kupitia habari, zinasababishwa na masuala
mbalimbali ikiwemo usalama wa wanahabari kuwa mashakani, mazingira
magumu ya kutekeleza majukumu yao, sheria za kuendesha vyombo vya
habari, weledi mdogo n.k
Nitajaribu kuelezea kwa ufupi namna ambavyo changamoto hizo
zinakwamisha maendeleo katika tasnia ya habari, kwa mfano usalama
mdogo kwa wanahabari unachangia kwa kiwango kikubwa kuua tasnia hii ya
habari kwa sababu utekwaji uteswaji na mauji yanayoendelea kuwakumba
wanahabari siku kwa siku kwakua wameandika au kutangaza habari
zinazowahusu watu wenye uwezo kifedha ni hali ambayo inafanya
wanahabari waogope kuandika habari zenye maslahi kwa taifa kwa kuhofia
maisha yao.
Mbali na taarifa za utafiti wa shirika la “Unesco” zinazoonesha
mwandishi wa habari mmoja anauawa kila wiki kote ulimwenguni, hapa
kwetu kuna mifano mingi ya kuthibitisha hilo.wandishi wa habari nchini
mwetu wameendelea kuteswa, kupigwa, kuharibiwa vitendea kazi,
kubambikiziwa kesi na hata kuuawa mbele ya jamii.
Wafuatiliaji wa vyombo vya habari wanafahamu kilichompata marehemu
Daudi Mwangosi katika kijiji cha nyololo wilayani mufindi kule Iringa
alikouawa kwa risasi na kuiacha familia yake ikihangaika isijue pa
kwenda akiwa katika utekelezaji wa majukumu yake ya kazi ya kutafuta
habari.
Jamii pia inafahamu yaliyomkuta mhariri mtendaji wa gazeti la
mwanahalisi Said Kubenea aliyemwagiwa tindikali machoni mnamo januari
sita 2008 akiwa katika utekelezaji wa majukumu yake ya kazi ofisini
kwake na mhariri mwenzake Ndimara Tegambwage aliyejeruhiwa kwa kukatwa
na mapanga kichwani.
Usiku wa kuamkia machi sita mwaka huu mwenyekiti wa jukwaa la wahariri
na mhariri mtendaji wa magazeti ya Habari corporation, Absalom Kibanda
naye akavamiwa usiku njiani akielekea nyumbani kwake maeneo ya mbezi
beach ambapo aliteswa, akapigwa na kung’olewa meno na kucha mpaka
akalazimika kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu zaidi.
Wapo wengi walio onja machungu ya fani ya uandishi wa habari akiwemo
Jerry Muro mtangazaji wa kituo cha shirika la utangazaji la Tanzania
TBC aliyedaiwa kuomba hongo ya shilingi za kitanzania milioni
kumi,Mungu saidia alionekana hana hatia baada ya kusota mda mrefu
vinginevyo hatujui nini kingeamliwa dhidi yake.
Kwa historia kama hii na kwakuwa mwandishi wa habari naye ni mwadamu
mwenye kuogopa mateso ya aina yoyote ikiwemo kifo na mengine mengi,
bila shaka ataogopa kuitaarifu jamii zile taarifa ambazo zinaweza
kuhatarisha maisha yake hata kama zitakuwa zina manufaa kwa taifa,kwa
sababu ameshuhudia wandishi wenzake waliojaribu kulipigania taifa lao
kwa kufichua uozo fulani waliishia kuteswa na kuambulia kifo.
Ijumaa ya wiki hii tumeshuhudia sherehe ya maazimisho ya siku ya uhuru
wa vyombo vya habari duniani kwa nchi za afrika mashariki yakifanyikia
mkoani Arusha huku yakihudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi wanachama
wa jumuia ya Afrika mashariki.maazimisho hayo yenye kauli mbiu isemayo
usalama na mazingira bora ya kufanyia kazi kwa wandishi wa habari
pamoja na mambo mengine pia utazinduliwa mfuko wa Daudi Mwangosi
unaolenga kumsaidia mwandishi wa habari baada ya kukumbwa na matatizo.
Hili ni jambo jema sana linalopaswa kuungwa mkono na watu wote wenye
nia njema na tasnia ya habari hapa nchini wakiwemo wandishi wa habari
wenyewe, lakini pamoja na nia njema ya jambo hili lisichukuliwe kuwa
ndio mwisho wa changamoto zinazo mkumba mwandishi wa habari na
kusababisha ashindwe kutekeleza wajibu wake mhimu kwa jamii.
Mfuko huo hata kama utajazwa mabilioni ya fedha ni vizuri wanahabari
wakafahamu kuwa hautaweza kumaliza kero zinazo mkabili mwandishi wa
habari, kwasababu mfuko unalenga kumsaidia mwandishi mara baada ya
kujeruhiwa au kupata matatizo mengine kama hilo, wakati akiendelea
kuwindwa na watenda maovu, akiendelea kunyonywa haki zake na mmiliki
wa chombo cha habari, akiendelea kubanwa na sheria kandamizi ikiwemo
sheria ya magazeti ya mwaka 1976 na nyinginezo, lakini pia akifanya
kazi katika mazingira magumu.
Kauli mbiu ya maazimisho hayo nayo haiwezi kuwa tiba ya matatizo kwa
wanahabari, ila inawatia moyo ili waendelee kuitumikia jamii huku
wakiendelea kuwindwa kama digidigi, na katika hili wanahabari lazima
wakubaliane wadai haki zao za msingi kwa kutumia kalamu zao ili
watekeleze wajibu wa kuziletea maendeleo jamii zao kwa kuandika habari
za ukweli zenye tija bila kuogopa ogopa mtu fulani kisa ana uwezo wa
fedha au nafasi aliyo nayo.
Vyombo vya habari kwa kiasi kikubwa ndivyo vyenye uwezo wa kuhamasisha
jambo lolote na likafanikiwa kwa haraka sababu wananchi wanaviamini na
vinanawafikia wananchi kwa haraka kuliko mawasiliano mengine, ndiyo
maana vinatumika na kufanikisha mambo muhimu yanayofanyika hapa nchini
kama vile chaguzi mbalimbali, sensa, chanjo, mikutano ya kisiasa,
kidini, n.k hivyo vinaweza kutumia ushawishi huo huo pasipo kuvunja
sheria za nchi ili mamlaka zinazohusika ziweze kusikia kilio chao.
Mamlaka zinazohusika, serikali na wamiliki wa vyombo vya habari lazima
ufike wakati watambue na kuuthamini mchango wa wanahabari katika
maendeleo ya jamii, na ni vyema wakatambua kuwa wanahabari wana uwezo
wa kufanya maamzi ambayo wataona yanawafaa ili kupata haki zao za
msingi zitakazo wawezesha kutekeleza majukumu ya kazi zao.japo
sishauri kugoma kutafuta na kutoa habari lakini ni vizuri serikali na
wamiliki wakajiuliza, hivi itakuwaje siku wanahabari wakiwagomea hata
kwa dakika chache tu!
Bila shaka kitatokea kitu kibaya sana ambacho hakijawahi kutokea na
dunia itatushangaa hakika.na kama hivyo ndivyo kuna umhimu mkubwa sana
kwa serikali kusikia kilio cha wanahabari kuhusu kubadirisha sheria
mbalimbali zinazo waongoza wanahabari na vyombo vyao, na pia kuna
umhimu kwa wamiliki wa vyombo vya habari kuwaboreshea wanahabari
mazingira bora ya kazi ikiwemo kuwalipa stahiki zao kwa wakati.
Na mwisho wanahabari wajitahidi kujiendeleza kitaaluma na kuhakikisha
kwamba wanakuwa na weledi wa kutosha katika utekelezaji wa majukumu
yao ili kuepuka kuandika mambo ambayo hayaendani na maadili ya
uandishi wa habari ikiwemo kuandika habari zisizo za kweli, au
kuandika habari kwa kuegemea upande fulani kutokana na kupokea rushwa
au vinginevyo.
Emmanuel Mkuwi
emmamkuwi@gmail.com
0715 015 560
No comments:
Post a Comment